Luke 23

Isa Apelekwa Kwa Pilato

(Mathayo 27:1-14; Marko 15:1-5; Yohana 18:28-38)

1 aKisha umati wote wa watu ukainuka na kumpeleka Isa kwa Pilato. 2 bNao wakaanza kumshtaki wakisema: “Tumemwona huyu mtu akipotosha taifa letu, akiwazuia watu wasilipe kodi kwa Kaisari na kujiita kuwa yeye ni Al-Masihi,
Al-Masihi maana yake ni Masiya , yaani Aliyetiwa mafuta.
mfalme.”

3 dBasi Pilato akamuuliza Isa, “Wewe ndiye mfalme wa Wayahudi?”

Isa akajibu, “Wewe wasema.”

4 ePilato akawaambia viongozi wa makuhani na watu wote waliokuwepo, “Sioni sababu ya kutosha kumshtaki mtu huyu!”

5 fLakini wao wakakazana kusema, “Anawachochea watu kwa mafundisho yake katika Uyahudi yote, tangu Galilaya alikoanzia, hadi sehemu hii!”

Isa Apelekwa Kwa Herode

6 gPilato aliposikia hayo akauliza, “Huyu mtu ni Mgalilaya?” 7 hAlipofahamu kwamba Isa alikuwa chini ya mamlaka ya Herode, akampeleka kwa Herode, ambaye wakati huo alikuwa pia Yerusalemu.

8 iHerode alipomwona Isa alifurahi sana, kwa sababu kwa muda mrefu alikuwa amesikia mambo mengi kumhusu yeye. Pia alitarajia kumwona akifanya miujiza kadha wa kadha. 9 jHerode akamuuliza maswali mengi, lakini Isa hakumjibu lolote. 10Wakati huo viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walikuwepo wakitoa mashtaka yao kwa nguvu sana. 11 kHerode na askari wake wakamdhihaki Isa na kumfanyia mzaha. Wakamvika vazi zuri sana, wakamrudisha kwa Pilato. 12 lSiku hiyo, Herode na Pilato wakawa marafiki; kabla ya jambo hili walikuwa na uadui kati yao.

Isa Ahukumiwa Kifo

(Mathayo 27:15-26; Marko 15:6-15; Yohana 18:39–19:16)

13 mBasi Pilato akawaita pamoja viongozi wa makuhani, viongozi wengine na watu, 14 nakawaambia, “Ninyi mlimleta huyu mtu kwangu kana kwamba ni mtu anayewachochea watu ili waasi. Nimemhoji mbele yenu nami nimeona hakuna msingi wowote wa mashtaka yenu dhidi yake. 15Wala Herode hakumwona na kosa lolote, ndiyo sababu amemrudisha kwetu. Kama mnavyoona, mtu huyu hakufanya jambo lolote linalostahili kifo. 16 oKwa hiyo nitaamuru apigwe mijeledi na kumwachia.” [ 17 pKwa kuwa ilikuwa lazima kuwafungulia mfungwa mmoja wakati wa Sikukuu.]

18 qNdipo watu wote wakapiga kelele kwa pamoja, “Mwondoe mtu huyo! Tufungulie Baraba!” 19(Baraba alikuwa amefungwa gerezani kwa sababu ya maasi yaliyokuwa yametokea mjini, na kwa ajili ya uuaji).

20Pilato, akitaka kumwachia Isa, akasema nao tena. 21Lakini wao wakaendelea kupiga kelele wakisema, “Msulubishe! Msulubishe!”

22 rKwa mara ya tatu, Pilato akawauliza, “Kwani amefanya kosa gani huyu mtu? Sikuona kwake sababu yoyote inayostahili adhabu ya kifo. Kwa hiyo nitaamuru apigwe mijeledi, na kisha nitamwachia.”

23Lakini watu wakazidi kupiga kelele kwa nguvu zaidi, wakidai kwamba Isa asulubiwe. Hivyo, kelele zao zikashinda. 24 sKwa hiyo Pilato akatoa hukumu kwamba madai yao yatimizwe. 25Akamfungua yule mtu aliyekuwa amefungwa gerezani kwa kuhusika katika uasi dhidi ya serikali na mauaji. Akamkabidhi Isa mikononi mwao, wamfanyie watakavyo.

Kusulubiwa Kwa Isa

(Mathayo 27:32-44; Marko 15:21-32; Yohana 19:17-27)

26 tWalipokuwa wakienda naye, wakamkamata mtu mmoja aitwaye Simoni mwenyeji wa Kirene, aliyekuwa anapita zake kuingia mjini kutoka shambani. Wakambebesha msalaba, wakamlazimisha auchukue nyuma ya Isa. 27 uIdadi kubwa ya watu wakamfuata Isa, wakiwamo wanawake waliokuwa wakimlilia na kumwombolezea. 28 vIsa akawageukia, akawaambia, “Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi bali jililieni ninyi wenyewe na watoto wenu. 29 wKwa maana wakati utafika mtakaposema, ‘Wamebarikiwa wanawake tasa, ambao matumbo yao hayakuzaa, wala matiti yao hayakunyonyesha!’ 30 xNdipo “ ‘wataiambia milima, “Tuangukieni!”
na vilima, “Tufunikeni!” ’

31 yKwa maana kama wamefanya hivi kwa mti mbichi, kwa mti mkavu itakuwaje?”

32 zWatu wengine wawili wahalifu, walipelekwa pamoja na Isa ili wakasulubiwe. 33Walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, hapo ndipo walipomsulubisha Isa pamoja na hao wahalifu, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wake wa kushoto. 34 aaIsa akasema, “Baba, wasamehe, kwa maana hawajui walitendalo!” Wakagawana nguo zake kwa kupiga kura.

35 abWatu wakasimama hapo wakimwangalia, nao viongozi wa Wayahudi wakamdhihaki wakisema, “Aliokoa wengine! Ajiokoe mwenyewe basi, kama yeye ndiye Al-Masihi wa Mungu, Mteule wake.”

36 acAskari nao wakaja, wakamdhihaki. Wakamletea siki ili anywe, 37 adna wakamwambia, “Kama wewe ni Mfalme wa Wayahudi, jiokoe mwenyewe.”

38 aeKwenye msalaba juu ya kichwa chake, kulikuwa na maandishi haya: Huyu ndiye Mfalme wa Wayahudi.

Maandishi haya yalikuwa yameandikwa kwa lugha za Kiyunani, Kilatini na Kiebrania.

39 afMmoja wa wale wahalifu waliosulubiwa pamoja naye akamtukana, akasema: “Wewe si ndiye Al-Masihi? Jiokoe mwenyewe na utuokoe na sisi.”

40Lakini yule mhalifu mwingine akamkemea mwenzake, akasema, “Je, wewe humwogopi Mungu, wakati uko kwenye adhabu iyo hiyo? 41 agSisi tumehukumiwa kwa haki kwa kuwa tunapata tunayostahili kwa ajili ya matendo yetu. Lakini huyu mtu hajafanya kosa lolote.”

42 ahKisha akasema, “Isa, unikumbuke utakapokuja katika Ufalme wako.”

43 aiIsa akamjibu, “Amin, nakuambia, leo hii utakuwa pamoja nami Paradiso.”
Paradiso maana yake bustani nzuri, hapa ina maana mahali zinapokwenda roho za wacha Mungu, yaani watakatifu.

Kifo Cha Isa

(Mathayo 27:45-56; Marko 15:33-41; Yohana 19:28-30)

44 akIlikuwa kama saa sita mchana, nalo giza likafunika nchi yote hadi saa tisa, 45 alkwa sababu jua liliacha kutoa nuru. Pazia la Hekalu likachanika vipande viwili. 46 amIsa akapaza sauti yake akasema, “Baba, mikononi mwako naikabidhi roho yangu.” Baada ya kusema haya, akakata roho.

47 anYule jemadari alipoona yaliyotukia, akamsifu Mungu, akasema, “Hakika, mtu huyu alikuwa mwenye haki.” 48 aoWatu wote waliokuwa wamekusanyika hapo kushuhudia tukio hili walipoyaona hayo, wakapigapiga vifua vyao kwa huzuni na kwenda zao. 49 apLakini wale wote waliomfahamu, pamoja na wale wanawake waliokuwa wamemfuata kutoka Galilaya, walisimama kwa mbali wakiyatazama mambo haya.

Maziko Ya Isa

(Mathayo 27:57-61; Marko 15:42-47; Yohana 19:38-42)

50 aqBasi kulikuwa na mtu mmoja mwema na mwenye haki, jina lake Yusufu. Yeye alikuwa mjumbe wa Baraza la Wayahudi,
Baraza la Wayahudi hapa ina maana ya Sanhedrin ambalo lilikuwa ndilo baraza la juu kabisa la utawala wa Kiyahudi, lililoundwa na wazee 70 pamoja na kuhani mkuu.
51 aslakini yeye hakuwa amekubaliana na maamuzi na vitendo vya viongozi wenzake. Huyu alikuwa mwenyeji wa Arimathaya huko Uyahudi, naye alikuwa anaungojea Ufalme wa Mungu kwa matarajio makubwa. 52Yusufu alikwenda kwa Pilato, akaomba apewe mwili wa Isa. 53Akaushusha kutoka msalabani, akaufunga katika kitambaa cha kitani safi, na kuuweka katika kaburi lililochongwa kwenye mwamba, ambalo halikuwa limezikiwa mtu mwingine bado. 54 atIlikuwa Siku ya Maandalizi, nayo Sabato ilikuwa karibu kuanza.

55 auWale wanawake waliokuwa wamekuja pamoja na Isa wakimfuata kutoka Galilaya wakamfuata Yusufu, wakaliona kaburi na jinsi mwili wa Isa ulivyolazwa. 56 avKisha wakarudi nyumbani, wakaandaa manukato na marhamu ya kuupaka huo mwili. Lakini wakapumzika siku ya Sabato kama ilivyoamriwa.
Copyright information for SwhKC